![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjKGugKIhe1yM5UqMlWVSBQ3MSghZfy3ySULRzqKlr96LRAq47udqofJZrCHOFi49evqXfQFN6PmSbFDuDUSwon12d8XLJTo_d5tK84C1iGX79zFplupWAadI8n9PWdIr1c8n_liMHN7OGa/w400-h395/IMG-20210205-WA0040.jpg)
Siku moja mwalimu mmoja wa secondary(high school) alitoa zoezi kwa wanafunzi wake na aliwaambia waandike watapenda kufanya kitu gani watakapokuwa wakubwa katika maisha yao. Wengi waliandika vitu mbalimbali, lakini kati yao alikuwepo mwanafunzi mmoja kwa jina la Monty Roberts ambaye yeye aliandika kuwa angependa aje kumiliki shamba la hekari 200 lenye ranchi ndani yake ambalo pia angelitumia kufundishia watu wengine mambo mbalimbali kuhusu farasi. Baada ya mwalimu kusahihisha mitihani, Mr.Monty alipata F na alipomuuliza mwalimu kwa nini amepata maksi hiyo alimwambia kuwa ni kwa sababu ndoto yake haina uhalisia kabisa(unrealistic). Akamwambia “wewe unatokea familia ninayoijua,ni maskini na hata wewe mwenyewe unajua huo mradi sio rahisi kuufanikisha. Utapata wapi pesa za kununua ardhi yote hiyo?utapata wapi pesa ya kununua farasi wa kisasa?” Jawabu ambalo Monty alimpatia mwalimu wake limeweka historia kubwa sana kuhusiana na masuala ya kuiamini ndoto kuelekea mafanikio. Baada ya mwalimu kumtaka Monty airudie ndoto yake ili iwe halisi kidogo alimjibu-“Keep your F,I will keep my Dream” akimaanisha-Bakia na F yako mimi nitaendelea kuiamini ndoto yangu. Hivi leo Monty anamiliki shamba la hekari 154 katika jiji la California, Marekani na anatoa mafunzo mbalimbali kwa watu wanaotaka kujifunza kuhusiana na mambo ya farasi kama ilivyokuwa ndoto yake. Katika kitabu chake maarufu cha “The man who listens to Horses”, Monty anawaita watu wanaofanana na yule mwalimu wake kama wezi wa ndoto(dream stealers),na anasema usikubali kuwasikiliza. Aina ya watu kama mwalimu wa Monty wako wengi sana na wako kila mahali. Watu hawa wanaweza kuwa wazazi wako,wanaweza kuwa marafiki zako,wanaweza kuwa wafanyakazi wenzako,anaweza kuwa mwajiri wako n.k. Kila wakati watakuwa wanakuambia “Hiyo ndoto ni kubwa sana,jaribu kuwa na ndoto ya kawaida”Katika kupitia hali hizi lazima utambue kuhusu mambo mawili makubwa: Moja ni kuwa watu hawa(dream stealers) ni wengi kuliko watu watakaokutia moyo(dream pushers) kwenye kuelekea mafanikio ya ndoto yako.Kila wakati utakapojaribu kufanya kitu fulani kisicho cha kawaida,watu wa namna hii watakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa katika maisha yako. Hii ni kawaida kwa sababu watu wengi huwa wanapenda kuona mnabaki katika hali zinazofanana.Hivyo usishangae ukikutana nao. Kila ndoto utakayojaribu kuitekeleza lazima utakumbana na watu wa namna hii katika maisha yako,watakuambia:Subiri uwe mkubwa,watakuambia ngoja kidogo,watakuambia haiwezekani,wat akuambia fulani alijaribu akashindwa n.k Pili ni lazima uwe na ujasiri wa kukabiliana nao. Inasikitisha kuona kuwa kuna watu wengi sana wamekata tamaa maishani mwao kwa sababu kuna watu waliwaambia kuwa ndoto yao haiwezekani ama mipango yao haitafanikiwa. Ni lazima uweke dhamira ya kutokubaliana nao wanapokukatisha tamaa-Kama bile monty alivyomwambia mwalimu wake-“Baki na F yako name nitabaki na Ndoto yangu”.Amua kumkabili kila anayekuambia haiwezekani kuwa “Baki na kutokuwezekana kwako,mimi ninabaki na ndoto yangu”. Mtu anapokuambia utafeli tu,uwe jasiri kumwambia-“Baki na kufeli kwako mimi ninaendelea na kuiamini ndoto yangu” Kufanikiwa kwa ndoto yako hakutegemei na idadi ya watu wanaoiamini ndoto yako bali inategemea wewe mwenyewe unaiamini kiasi gani bila kujali kuna watu wangapi ambao hawaiamini. Kuanzia leo,weka azimio kuishi kama Mr.Monty,kwa kila utakayekutana naye na akakukatisha tamaa katika kuielekea ndoto yako,amua kutokubaliana naye. Ninaamini wale ambao leo wanakuambia ndoto yako haiwezekani wataishi miaka mingi na watashuhudia ndoto yako ikitimia. IAMINI NDOTO YAKO ZAIDI KULIKO UNAVYOAMINI MANENO YA WASIOIAMINI NDOTO YAKO. Kumbuka kuwa ndoto yako Inawezekana. Anza sasa kuelekea kuitimiza ndoto yako
0 Maoni