Jinsi ya Kujikwamua kiuchumi kwa Ufugaji wa Kuku wa Kienyeji

Kila siku mwanadamu yupo vitani akipambana na maisha yake, kwamba ni namna gani atakomboka kiuchumi. Mbinu mbalimbali hutumika ili kufikia malengo ya kushinda mapambano hayo ambayo sio siri kwamba hayahitaji kurudi nyuma ila kupiga moyo konde.
Ni vita kubwa na nzito kweli ambayo muamuzi wake huwa ni kifo kutokana na ukweli kuwa katika maisha yote, mwanadamu huhitaji uchumi imara pasipo kujali ukubwa wake kwa kuwa hutegemea aina ya ngazi pamoja na kundi linalomfuata.
Hitajio la uchumi wa mtu mmoja halifanani na la watu watatu. Bajeti ya ngazi ya familia haiwiani na ya nchi nzima. Lakini zote zinalenga kujenga uchumi ingawaje misheni zake zinatofautiana kwa kiasi kikubwa kutokana na michakato ya kufikia malengo.
Karibu masuala yote ya mwanadamu yanahitaji uchumi tena imara, kinyume chake ataishia kudhalilika na kusimangwa katika jamii inayomzunguuka jambo ambalo hakuna anayelifurahia.
Ni ajabu kwa mwenye akili timamu akahiyari kuwa omba omba pasipo kuona haya mbele za watu. Kinachopelekea kufikia hatua ya kuomba ni uhitaji wa jambo ambalo kwa wakati huo yeye hanalo na hana jinsi zaidi ya kujikwangua uso kuondoa soni kuomba.
Kuomba kunadhalilisha kiasi cha kuwaogopesha wengine hata kuamua ‘kufa kizungu tai shingoni.’ Maana huko kukutana na majibu ya kebehi, dharau, kuudhi au kutukanwa ni jambo la kwaida sana.
Kudanganywa, kunyamaziwa au kukimbiwa na anayelengwa kuombwa hasa akiwa na taarifa au kufahamu ujio wa muombaji ni sehemu ya malipo ya kuomba. Mwanadamu anayejitambua huwa hapendi kukutana na madhila haya na mengine kibao yanayoambatana na tabia ya kuomba.
Kwa kweli haipendezi kuinua kinywa kuomba, lakini shida nazo hazina utatuzi zaidi ya uchumi imara ambao umeota mbawa sio kwa nchi tu bali hata kwa wananchi wake kiasi kinachopelekea kukokosa mbadala wa kujinusuru zaidi ya kuomba.
Si kula, kuvaa, kulala wala kujitibu, kote kunahitaji nguvu ya uchumi. Na bahati mbaya hakuna shughuli yoyote inayoitwa ya kiuchumi isiyogusa pesa ambayo ndiyo mhimili mkubwa katika uchumi wa mtu mmoja-mmoja na nchi kwa ujumla. Kila siku pesa husakwa kwa udi na uvumba.
Na ndio maana kilio cha kila mmoja leo hii ni pesa kwa kuwa anajua kuwa atanunua na kuuza, atalima na kuvuna, atamiliki ardhi na majengo mbalimbali, atasoma au kusomesha na kufanya mambo kadha wa kadha iwapo atakuwa nayo.
Lakini kuadimika kwa pesa kusiwe chanzo cha kukata tamaa katika uwanja wa vita. Kusichochee kujilemaza kwa kila mmoja kuwa ombaomba wa kudumu kwa sababu atakosekana wa kumsaidia mwingine mbali ya kudhalilika. Badala yake kuamshe mori wa kuisaka mchana na usiku, iwe mvua au jua.
Kwamba katika mbio za kiuchumi, kila mmoja humtegemea mwenzake kwa namna moja au nyingine. Mathalani, mvuvi humtegemea mchuuzi au mlaji wakati mwalimu humtegemea mwanafunzi ilhali serikali inategemea wananchi, na kadhalika.
Lakini jambo kubwa kwa mtu mmoja-mmoja, na kwa makundi, ni kuhiyari kutafuta mlango wa kutokea ili waweze kujinasua katika vita ya uchumi. Badala ya kuinua mikono juu kusalimu amri na mwishowe kuwa tegemezi kwa sura ya ombaomba, ni kupigana kiume kuishinda vita ya uchumi.
Alama ya kuishinda vita hiyo ni pale kila mmoja anapoweza kukidhi mahitaji yake ya muhimu na hata ya ziada pasipo kujidhalilisha kwa kupitisha bakuli la kuomba kila uchao na uchwao kiasi kinachoweza kupelekea kuchokwa, kukimbiwa na hata kupewa maneno yasiyo na utu.
Na hili linawezekana kwa jambo moja tu la uthubutu wa kuupigania uchumi imara kuanzia ngazi za chini. Kwamba kila mmoja, kwa nafasi yake, akiamua kuwa mbunifu wa jambo au shughuli itakayomkomboa kiuchumi pamoja na waliomzuguuka, itasaidia kuishinda vita hii.
Na sio tu kubuni bali hata kujifunza au kuiga shughuli za kiuchumi kutoka kwa wengine na kisha kuamua kuifanya kwa kadiri ya uwezo wa mtu au kikundi kunatosha kuondoa udhalili wa kuombaomba hasa kwa mahitaji ya kawaida.
Moja ya shughuli zinazoweza kusaidia katika vita ya kiuchumi na kupelekea watu kuacha tabia dhalili ya kuombaomba ni ufugaji bora wa kuku wa kienyeji. Kuku wa kienyeji huhimili magonjwa na hujitafutia wenyewe chakula wanapoachwa huru.
Kuku hawa wanaatamia mayai, wanatotoa na kulea vifaranga vyao, na ni wepesi kujilinda na maadui zao kuliko kuku wa kisasa. Pia kuku wa kienyeji hustahamili mazingira magumu kama vile mahali pakame na penye baridi.
Katika jamii inayotuzunguuka wapo wafugaji wa kuwapigia mfano kutokana na kunufaika kwa shughuli hii ya ufugaji bora wa kuku hawa. Wengine ni ndugu au marafiki wa karibu kabisa ambao hushirikiana nao katika masuala kadhaa ya kijamii.
Wafugaji hawa hawana shida tena ya kuzurura huko na kule kutembeza bakuli la kutaka kusaidiwa pesa kwa ajili ya chakula, mavazi, malazi na maradhi. Hawasumbuki kuhaha kuomba kwa ajili ya kusomesha au kusoma wao wenyewe na wengine wanamiliki usafiri binafsi.
Kifupi ni kwamba wafugaji hawa wameingia kwenye orodha ya wasiokuwa ombaomba na baadhi yao wanawasaidia waliokata tamaa ya kupigana vita ya uchumi na kuhiyari kujidhalilisha kwa kutembea kila kukicha mitaani, misikitini na maeneo mengine kuomba.
Ingawa wengine, kutokana na hali zao na jamii iliyozunguuka, hawana jinsi ila kusubiri msaada ikiwa ni pamoja na kuomba, lakini kuna kundi kubwa lenye uwezo wa kupambana limehiyari kujikatia tamaa na kujiingiza kwenye orodha ya wasiojiweza kwa chochote.
Kunahitajika elimu ya hali ya juu pamoja na ushawishi ili kuliondoa kundi hili katika maisha ya utegemezi na udhalili. Wanahitaji kuoneshwa kwa macho yao namna ya kuachana na mawazo mgando ya kuombaomba au kulala nyumbani kusubiri ajira.
Moja ya njia za kuwakomboa ni ufugaji bora wa kuku wa kienyeji, na ni vema wakaona jinsi wale waliothubutu kuwekeza katika ufugaji huo walivyotononoka. Wapelekwe wakawaone wenzao tena miongoni mwao wapo wenye elimu zaidi yao, namna wanavyoupungia mkono wa kwaheri umasikini kupitia ufugaji.
Upi Ufugaji bora wa kuku wa kienyeji?
Awali ni lazima tukiri kuwa wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji huwafuga kienyeji kama lilivyo jina lenyewe. Kwamba wanafuga kuku kwa mazowea kama vile urithi tu toka kwa wazee wetu na sio kuwatumia kuku hao kama moja ya nyenzo ya kujinasua kiuchumi.
Wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji hawana muda wa kutafuta maarifa ya ufugaji bora. Hawana chochote cha kuzingatia zaidi ya kujua ana kuku wangapi, ametaga mayai mangapi na ametotoa vifaranga vingapi, basi.
Hawajui kama kuku wa kienyeji ni moja ya vyanzo vizuri vya mapato hasa endapo watafugwa kwa kuzingatia kanuni na maelekezo ya ufugaji bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha makazi/mabanda bora ya kuku, chakula, tiba na kinga za magonjwa ya kuku.
Baadhi ya wafugaji twakiwemo wale waliojizatiti kutumia miradi ya ufugaji kupambana na umasikini bado hawazingatii usafi wa mabanda pamoja na vyombo wanavyowekea chakula au maji ya kuku.
Jambo kubwa la kuzingatia kwa wafugaji wa kuku ni kuwa na ukaribu na wataalamu wa mifugo. Hawa watasaidia mno sio tu kupata kuku kwa ajili ya kitoweo na mayai bali kuwa chanzo kimojawapo cha mapato jambo litakalosaidia kupunguza idadi ya ombaomba.
Ingawa ufugaji bora wa kuku wa kienyeji unahitaji gharama fulani, lakini ni bora kuomba kusaidiwa ili kukamilisha mradi wa ufugaji kuliko kuendelea kuomba kila kukicha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kawaida.

Chapisha Maoni

0 Maoni